Wednesday, February 4, 2009

Serikali yaomba bunge fedha za EPA

Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo amewasilisha bungeni muswada wa nyongeza bajeti ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2008/09 iliyoidhinishwa na bunge Juni mwaka jana.

Katika muswada huo serikali imeliomba bunge kuidhinisha matumizi ya kiasi cha
Sh53 bilioni zilizorudishwa na kampuni zilizozichota fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ili zitumike katika bajeti yake ya mwaka 2008/09.

Iwapo muswada huo utapitishwa bajeti ya serikali kwa mwaka 2008/09 itakuwa ni jumla ya Sh7.273 trilioni tofauti na ile iliyoidhinishwa awali ya Sh7.22 trilioni.

Mchanganuo wa bajeti hiyo ya nyongeza unaonyesha kwamba kiasi cha Sh3 bilioni zitapelekwa Hazina, Sh10 bilioni Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Sh40 bilioni Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Fedha zitakazoenda Hazina ni kwa ajili ya kuongeza mtaji wa Benki ya Raslimali (TIB) na zitakazoenda Wizara ya Mifugo na Uvuvi zitasaidia kugharimia dawa za mifugo wakati zitakazopelekwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika zitagharimia pembejeo za kilimo.