Wednesday, March 4, 2009

Polisi yawashikilia wanafunzi wawili Udom

Wanafunzi wakiwa katika moja ya matukio ya migomo katika chuo kikuu cha Dodoma katika picha hii ya maktaba.....

Polisi mjini Dodoma leo imethibitisha kuwakamata wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuhusiana na mgomo uliotokea Jumanne wiki hii chuoni hapo.


Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma (RPC) Omary Mganga amewaambia waandishi wa habari kuwa wanafunzi hao wanaweza kufikishwa mahakamani uchunguzi wa polisi ukikamilika. Hata hivyo alisita kutaja majina ya wanafunzi hao pamoja na makosa ambayo huenda wakashitakiwa dhidi yao.


Amesema kuwa polisi bado inaendelea kukusanya vielelezo juu ya tukio hilo ambapo wanafunzi wanaosoma masomo ya ualimu walifanya maandamano kushinikiza madai yao ikiwamo kulipwa fedha za mkopo wa elimu zinazotolewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu.


Uharibifu mdogo ulifanywa na wanafunzi hao ikiwemo kuharibu milango ipatayo tisa na kumjeruhi mwangalizi mmoja wa mabweni yao.


Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia Mipango Fedha na Utawala Profesa Shabaan Mlacha amesema kuwa bado kamati ya watu watano iliyoundwa kuchunguza vinara wa mgomo huo inaendelea na kazi yake.


Polisi ililazimika Jumanne wiki hii kufyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi hao ambao walikuwa wakiandamana kutoka katika kampasi yao eneo la Ng’ong’ona kuelekea jengo kuu la Utawala lililopo Chimwaga.

Utatuzi wa migogoro

Mbunge wa Same Mashariki,Anna Kilango Malecela(katikati) akiwaongoza mamia ya wanawake wa jamii ya wafugaji wilayani Same juzi, kutoa tamko linalotaka kutumika kwa njia za kijadi kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji badala ya matumizi ya nguvu.Kushoto kwake ni kijana wa Kimasai, Kipintu Sany aliyejeruhiwa wiki mbili zilizopita katika mapigano ya wafugaji na wakulima. Picha ya Daniel Mjema

Bongo wakati mwingine .... Utalijua jiji....!!!

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu (katikati) na rafiki yake Asha Jumbe wakisindikizwa na askari polisi wakielekea kupanda basi la Magereza kuelekea rumande.


Hapa wakiwa ndani ya basi hilo kabla ya kuelekea rumande..... Picha za Kuruthum Ahmed

Deus Malya ajitetea...

Katika Picha hii ya Maktaba anaonekana Deus Malya (kulia) akiwa na wakili wake wakati kesi yake inayoendelea mjini Dodoma. Leo yaliyojiri ndo kama haya......... endelea.....

Mahakama mjini Dodoma imepanga Ijumaa ya wiki hii kuwa ni siku ya mwisho ya kufunga ushahidi kwa kesi dhidi ya Deus Malya aliyekuwamo katika gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe.

Hakimu Mfawidhi, Thomas Simba amekubali ombi la upande wa utetezi na mashitaka kwa mahakama kupanga tarehe ya kufunga kesi hiyo kabla ya mahakama kutoa hukumu.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amekubali uamuzi wa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Godfrey Wasonga huku upande wa mashitaka chini ya mwendesha mashitaka wa serikali Neema Mwanda ukiomba kuwasilishwa kwa ufungaji wa kesi hiyo matamshi na sio maandishi ili kuokoa muda.

Akitoa Utetezi wake jana mbele ya Hakimu Simba, Malya amekanusha kuendesha gari lililopata ajali tarehe 28 mwezi Julai mwaka jana na kusababisha kifo cha marehemu Wangwe.

Akijitetea Malya, ambaye alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Umbwe na baadaya kuendelea na masomo ya sekondari na ngazi ya chuo katika chuo cha Mtakatifu Herbert Nairobi Kenya , alisema kuwa hayawahi kuendesha gari, na wala yajawahi kupata ajali ya gari kabla ya hiyo ya Julai 28 mwaka jana.

Akiongozwa na wakili wake, Malya alipinga ushahidi uioltolewa mahakamani na mashahidi nane waliololetwa na upande wa mashitaka huku akiunga mkono ushahidi wa shahidi wa tisa uliotolewa na mtaala kutoka Taasisi ya Usafirishaji ya Taifa.

Malya aliieleza mahakama kuwa ushahidi uiliotolewa mashahidi hao nane hauthibitishi kuwa yeye alikuwa akiendesha gari hilo aina ya Toyota Collora lenye namba za usajili T865 ARM.

Ajali hiyo iliyokea majira ya saa mbili na nusu usiku katika barabara ya Dodoma-Morogoro eneo la Pandambili, Wilayani Kongwa takriban umbali wa kilometa 120 kutoka mjini Dodoma wakati yaye na marehemu Wangwe wakiwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam.

Malya anashitakiwa kwa makosa mawili katika kesi namba TR 103 ya mwaka 2008 ambayo ni kuendesha kwa mwendo kasi na kusabisha ajali pamoja na kuendesha gari bila ya kuwa na leseni ya udereva.

Malya aliunga mkono ushahidi wa mtaalam kutoka NIT uliothibitisha kuwa gari hilo lilikuwa na kasoro katika gurudumu lake kwa kuwa lilikuwa limeongezwa urefu kwa takriban inchi moja jambo ambalo limengeweza kusababisha gurudumu hilo kupasuka na kusababisha ajali.

Amesema maelezo ya mtaalam huyo yanakinzana na ripoti ya mkaguzi wa gari kutoka idara ya usalama barabarani ambaye aliiambia mahakama kuwa gari hilo halikuwa na ubovu wowote kabla ya ajali.

Malya aliyedai kuwa na umri wa miaka 25 tofauti na ilivyoandikwa kwenye hati ya mashitaka kuwa na umri wa miaka 27 alisema kuwa hati hiyo ya mashitaka inamtaja yeye kuwa na dereva na mfanyabiashara jambo ambalo sio la kweli kwani yeye hamiliki leseni ya udereva na wala hajawahi kuendesha gari.

Kwa mara kadhaa upande wa Mashitaka ulimuomba hakimu kutomruhusu wakili wa utetezi kuuliza maswali yanayolenga kutoa mwelekeo wa majibu ya mteja wake, jambo ambalo hakimu Simba alilitolea ufafanuzi.

Kwa muda mwingi wa utetezi wake, Malya aliieleza mahakama juu ya mashaka aliyonayo katika ushahidi uliotolewa dhidi yake huku akidai kuwa vielelezo kadhaa vilivyowasilishwa mahakamani hapo vinamapungufu.

Malya alieleza mahakama kuwa ripoti mbili zinakinzani kutokana na ukweli kwamba ripoti ya uchunguzi wa maini na figo za marehemu iliyosainiwa na mkemia mkuu inaonyesha kuwa alikuwa amemeza dawa za malaria tofauti na ile ya hospitali ya taifa ya muhimbili ambayo ilionyesha tofauti.

Malya pia amedai mahakamani hapo kuwa ripoti ya mkemia inaonyesha kuwa uchunguzi wa maini na figo za marehemu ulifanywa tarehe moja mwezi Januari mwaka jana, muda ambao marehemu Wangwe alikuwa bado yu hai.

Hata hiyo Hakimu Simba alisita kuruhusu ripoti hiyo kutumika kwa wakati huo katika mahojiano kwani ilipokelewa mahakamani hapo wakati wa usikilizaji wa awali wa kesi hiyo kama kielelezo kisichokuwa na pingamizi.

Kesi hiyo ambayo imevuta hisia za wakazi wengi wa Dodoma , Hakimu Simba pia alitoa maelekezo mara kadhaa juu ya utaratibu wa utetezi wa tafsiri kadhaa za masuala yaliyojitokeza mahakamani hapo.

Malya aliieleza mahakama kuwa alimfahamu Marehemu Wangwe kupitia baadhi ya viongozi wa Chadema ambao amekuwa akiwafanyia kazi zao kadhaa zihusianazo na uchapishaji na ubunifu wa maandishi na michoro.

Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza alimfahamu marehemu Wangwe mwaka 2005 wakati alipomfanyia kazi ya kubuni na kutengeneza vipeperushi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi na pia fulana kwa ajili ya kutunisha mfuko kwa ajili ya maendeleo ya jimbo la Tarime.

Malya aliieleza mahakama kuwa alifika mjini Dodoma baada ya kuitwa na marehemu Wangwe kwa ajili ya kazi ya kuhariri na ubunifu wa maandishi wa kitabu chake kilichokuwa na jina la “Hii si Demokrasia”.

Siku hiyo ya ajali, alieleza kuwa walianza safari majira ya saa moja usiku na baada ya kutoka nje kidogo ya mji, walisimama ambapo marehemu alikwenda kununua kadi ya muda wa maongezi wa simu ya mkononi.

Alisema marehemu alimsihi akae katika kiti cha nyuma ili aweze kulala kwani alikuwa anajisikia usingizi, jambo ambalo alikubali na kwenda kukaa kiti cha nyuma ya dereva na kufunga mkanda wa usalama katika gari.

“Baada ya kwenda mwendo mrefu kidogo, ghafla nilisikia marehemu akisema hayaaaa…..!! na mara gari likaanza kubingirita na baada ya kutulia ndipo nikashituka kuwa tumepata ajali,” alieleza Malya.

Alipoulizwa na Hakimu, Malya alieleza kuwa mwili wa marehemu wangwe ambaye alidai kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari huku hajafunga mkada wa usalama garini ukiwa umelala sehemu ya mbele ya gari, miguu yake ikiwa upande wa dereva wakati sehemu nyingine za mwili zikiwa upande wa pili huku koti lake likiwa limebanwa.

Ubishani mdogo ulizokuwa unatokea wakati wa mahojiano baina ya Malya na upande wa mashitaka ambao ulimtaka mshtakiwa huyo kujibu Ndiyo ama Hapana kwa maswali aliyokuwa akiulizwa huku Malya akitaka kutoa ufafanuzi wa hayo aliyokuwa akiulizwa.