Katika mabadiliko hayo, amewateua Wakuu wa Mikoa wapya 15, kuwabadilisha vituo vya kazi Wakuu wa Mikoa watano na wengine saba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu. Mkuu wa Mkoa wa Singida amebaki kwenye kituo chake cha kazi wakati Wakuu wa Mikoa wengine wanne watapangiwa kazi nyingine.
Aidha, Wakuu wa Mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Wakuu wa Wilaya 11 wamepandishwa Vyeo na kuwa Wakuu wa Mikoa kama ifuatavyo: Bw. John Gabriel Tupa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara; Bw. Saidi Thabit Mwambungu (Ruvuma); Bi. Chiku S. Gallawa (Tanga); Bw. Leonidas T. Gama (Kilimanjaro); Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma); Bw. Elaston Mbwillo (Manyara); Kanali Fabian Massawe (Kagera); na Bibi. Fatma Abubakar Mwassa (Tabora). Wakuu wa Wilaya wengine walioteuliwa ni Bw. Ali Nassoro Rufunga, (Lindi); Eng. Ernest Welle Ndikillo, (Mwanza); na Bw. Magesa Stanslaus Mulongo Mkuu wa Mkoa (Arusha).
Walioteuliwa nje ya nafasi hizo ni Eng. Stella Manyanya (Rukwa); Bibi Mwantumu Mahiza, (Pwani); Bw. Joel Nkaya Bendera (Morogoro) na Bw. Ludovick Mwananzila (Shinyanga).
Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Bw. Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza; Bw. Said Mecki Sadiki anayekwenda Dar es Salaam akitokea Lindi; Bibi Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma; Lt. Kanali Issa Machibya anayekwenda Kigoma akitokea Morogoro; na Kanali Joseph Simbakalia anayekwenda Mtwara akitokea Kigoma. Dk. Parseko Ole Kone ataendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Waliostaafu ni Bw. Mohammed Babu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera; Bw. Isidore Shirima aliyekuwa Arusha; Kanali (mst.) Anatory Tarimo aliyekuwa Mtwara; Bw. John Mwakipesile, aliyekuwa Mbeya. Wengine ni Kanali Enos Mfuru aliyekuwa Mara; Brig. Jen. Dk. Johanes Balele aliyekuwa Shinyanga; na Meja Jen. Mst. Said S. Kalembo aliyekuwa Tanga.
Wakuu wa Mikoa wanne waliostaafu ambao watapangiwa vituo vingine vya kazi ni Bibi Amina Mrisho aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani; Dk. James Msekela aliyekuwa Dodoma; Bw. Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Bw. Daniel Ole Njoolay aliyekuwa Rukwa.
Wakuu wote wa Mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa Hati za Makabidhiano (Handing Over Notes) katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa kwa Wakuu wapya wa Mikoa. Aidha Wakuu wa Wilaya ambao wamepandishwa vyeo kuwa Wakuu wa Mikoa nao wanapaswa kufanya hivyo hivyo kwa ajili ya Wakuu wa Wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na uteuzi wao.
Wakuu wa Mikoa ile minne mipya na Wakuu wa Wilaya watakaoteuliwa hapo baadaye nao watatakiwa kuandaa Hati za Makabidhiano ndani ya siku 14 tangu kuapishwa.
Makabidhiano hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao.
Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa na Wakuu wa Mikoa minne mipya wakaoteuliwa pamoja na Wakuu wote wa Wilaya watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika watatakiwa kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu kwenye Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.
Wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa siku ya Ijumaa, Septemba 16, 2011 saa 4.00 asubuhi kwenye viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wakuu hao wapya wa mikoa; vituo wanavyokwenda na vituo walivyotoka ni kama ifuatavyo: