Tuesday, May 25, 2010

Tanesco yapata bosi mpya

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imemteuwa Mhandisi William Geofrey Mhando kuwa Mkurugenzi mpya wa TANESCO. Uteuzi huo unaanza rasmi Juni 1, 2010.

Taarifa iliyotolewa jana (Jumanne) na Idara ya Mawasiliano ya Tanesco imeeleza kuwa Kabla ya uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji umeme na Masoko katika shirika hilo.

Mhando anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Dr. Idris Rashid ambaye muda wake wa uongozi katika shirika hilo umemalizika.

Mhando aliajiriwa na TANESCO October 1987 kama Mhandisi wa umeme, ambapo baadaye alipandishwa na kuwa Mhandisi katika line za umeme.

Mwaka 1990 hadi 1992 aliteuliwa kuwa Meneja wa TANESCO mkoa wa Singida ambapo baadaye mwaka 1992 hadi 1994 alikuwa Meneja wa mkoa wa TANESCO mkoa wa Mbeya.

Vilevile alipandishwa cheo mwaka 1995 na kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini Magharibi hadi mwaka 1999.

Aidha, Mhandisi Mhando ana elimu ya Shahada ya Uzamili (Masters) katika masuala ya umeme aliyoipata Havana Cuba mwaka 1987, vile vile ana elimu aliyoipata katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Gari ya JK yabuma wakati wa msafara

Cruiser zilizokuwa zimembeba JK wakati wa ziara yake jumatatu jijini Dar zilibuma maeneo ya BP, Kilwa road(pichani juu) na maeneo ya Kimara, Morogoro road(pichani chini)... (picha kwa hisani ya mdau Michael Jamson)....soma habari zaidi hapo chini......
Gari la JK lazima ghafla barabarani
Tuesday, 25 May 2010 09:33
ZIARA ya Rais Jakaya Kikwete aliyoifanya jana mkoani Dar es Salaam ilipata mushkeli baada ya gari alilotumia kwenye msafara wake kuzimika ghafla mara mbili barabarani.

Gari hilo lilizimika kwa mara ya kwanza katika makutano ya barabara ya Morogoro na Mavurunza wilayani Kinondoni eneo la Kimara Mwisho majira ya saa 7:30 mchana ambako msafara wake ulisimama kwa dakika tatu.

Gari hilo lilizimika tena kama hatua 150 tu kutoka katika makutano hayo na ndipo rais akahamishiwa kwenye gari lingine lililokuwa kwenye msafara huo huku akiwa ananyeshewa mvua.

Tena majira ya saa 10:00 jioni msafara wake uliokuwa ukitokea Keko Toroli wilayani Temeke, ulikwama tena maeneo ya BP barabara ya Kilwa ambako gari hilo jipya nalo lilizimika ghafla.

Tukio hilo la kihistoria nchini, liliwapa wakati mgumu maafisa usalama ambao kila mara gari lilipokuwa limezimika, walishuka kwenye magari yao na kuondoa bendera na ngao.

Kusimama gafla kwa msafara wake eneo la Kimara, kulimlazimisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Mark Mwandosya kukimbilia eneo alilokuwapo rais huku umati wa watu uliokuwa umejibanza pembeni mwa barabara nao ukisogea karibu.

Ilimchukua takriban dakika mbili kwa maafisa wa usalama wa taifa kupata suluhu ya namna msafara huo utakavyoendelea kutokana na mkanganyiko wa gari ipi kati ya mbili zilizokuwa zinafanana aiangie rais.

Msafara huo uliendelea baada ya Rais Kikwete ambaye alikuwa amevaa shati la kitenge la mikono mirefu na akiwa analowa hasa miguuni kuhamishiwa katika gari jingine huku lile lililoharibika likiwa linasukumwa na umati wa watu hadi pembezoni mwa barabara.

Hata hivyo, baada ya dakika nane gari hilo aina ya Toyota Landcruiser VX V8 lililokuwa na rangi nyeusi, liliwaka baada ya dereva kujaribu kuliwasha kwa zaidi ya mara nne.

Kuzimika kwa gari lake eneo la PB kulifanya msafara wa rais usimame kwa takriban dakika kumi kabla ya kuendelea hadi Ikulu ambako alipumzika kwa muda na kuenda ukumbi wa Karimjee kufanya majumuisho ya ziara yake.
Source: http://mwananchi.co.tz