Tuesday, January 27, 2009

Mramba ndani ya bunge


MBUNGE wa jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro ambae anatuhumiwa kwa kesi ya kutumia vibaya madaraka yake akiwa waziri wa fedha Basili Mramba jana aliingia katika ukumbi wa bunge kwa mbwembwe huku wabunge wakionekana kumpa pole na kumkumbatia kila wakati.

Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja iwapo amri ya mahakama iliyomruhusu kwenda kutembelea jimbo lake pia inampa nafasi ya kuhudhuria bungeni.

Mramba aliingia katika ukumbi wa bunge majira ya saa 2:46 asubuhi akiongozana na Waziri wa fedha Mustafa Mkulo aliingia huku baadhi ya wabunge walipomuona walianza kumfuata na kukumbatiana katika hali iliyoonyesha kuwa walikuwa wakimpa pole kwa masahibu yaliyomkuta.

Alipoingia katika ukumbi huo alisimama kwa muda mrefu mlangoni ikwa ndani akizungumza na Benedict Ole-Nangoro ambae ni mbunge wa Kiteto (CCM) huku baadhi ya wabunge wengi wa ccm wakipita na kusalimiana nae na kukumbatiana kwa kila mtu.

Katika hali hiyo haikuweza kufahamika mara moja Mramba na Ole-Nangoro walikuwa wakizungumza kitu gani kwa muda mrefu mlangoni hapo hadi mazungumzo yao yalipokatizwa na sauti iliyoashiria kuwa Spika wa bunge alikuwa anaingia katika ukumbi huo.

Ole-Nangoro ni mmoja wa wabunge walioingia katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuziba nafasi za wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kiteto Benedict Losulutya mwishoni mwa mwaka 2007 na hivyo sio mbunge wa siku nyingi katika bunge hilo.

Mbunge huyo wa Rombo inasemekana alipewa kibali na Mahakama kwa kutembelea jimbo lake na hata kuhudhuria vikao vya bunge akiwa bado ni mbunge halali wa jimbo hilo ingawa kesi yake bado iko Mahakamani.

Haikuweza kufahamika mara moja ni kwa nini mbunge huyo aliweza kufuatwa na wabunge wengi kutoka katika chama chake (ccm) na kusalimiana nae ingawa dalili zilionyesha kuwa kulikuwa na hali ya kupeana pole na kumuweka katika hali ya ujasiri zaidi katika kesi inayomkabili.

Wakati wa mchana mbunge huyo alitoka katika ukumbi wa bunge mnamo saa 7:03 akiwa amefuatana na naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano Anna Makinda huku hali ya kumfuata na kusalimiana nae Mramba ikiwa ni ileile kama aliyoingia nayo asubuhi.

Mramba anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake akiwa waziri wa fedha wakati wa utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamini Mkapa na kwamba alifikishwa mahakamani pamoja na aliyekuwa waziri wa nishati na madini kwa wakati huo Daniel Yona ambae pia amewahi kuwa waziri wa fedha.

No comments: