Wednesday, March 4, 2009

Polisi yawashikilia wanafunzi wawili Udom

Wanafunzi wakiwa katika moja ya matukio ya migomo katika chuo kikuu cha Dodoma katika picha hii ya maktaba.....

Polisi mjini Dodoma leo imethibitisha kuwakamata wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuhusiana na mgomo uliotokea Jumanne wiki hii chuoni hapo.


Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma (RPC) Omary Mganga amewaambia waandishi wa habari kuwa wanafunzi hao wanaweza kufikishwa mahakamani uchunguzi wa polisi ukikamilika. Hata hivyo alisita kutaja majina ya wanafunzi hao pamoja na makosa ambayo huenda wakashitakiwa dhidi yao.


Amesema kuwa polisi bado inaendelea kukusanya vielelezo juu ya tukio hilo ambapo wanafunzi wanaosoma masomo ya ualimu walifanya maandamano kushinikiza madai yao ikiwamo kulipwa fedha za mkopo wa elimu zinazotolewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu.


Uharibifu mdogo ulifanywa na wanafunzi hao ikiwemo kuharibu milango ipatayo tisa na kumjeruhi mwangalizi mmoja wa mabweni yao.


Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia Mipango Fedha na Utawala Profesa Shabaan Mlacha amesema kuwa bado kamati ya watu watano iliyoundwa kuchunguza vinara wa mgomo huo inaendelea na kazi yake.


Polisi ililazimika Jumanne wiki hii kufyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi hao ambao walikuwa wakiandamana kutoka katika kampasi yao eneo la Ng’ong’ona kuelekea jengo kuu la Utawala lililopo Chimwaga.

No comments: