Friday, January 23, 2009

Chadema kuwasilisha hoja binafsi bungeni

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeeleza nia yake ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi inayolenga kuilazimisha serikali kuhakikisha hakuna mtoto atakayekosa fursa ya kusoma kwa sababu ya umasikini wa wazazi wake.

Hatua hiyo ya Chadema imekuja huku wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakipinga mchakato wa kudahili wanafunzi upya baada ya vyuo vikuu kufunguliwa.

Katika taarifa yake iliyoitoa jana jijini Dar es Salaam, Chadema imeeleza kusikitishwa kwake na utaratibu wa kudahili upya wanafunzi wa shahada ya kwanza unaoendelea UDSM kutokana na kile ilichokieleza kuwa utaratibu huo ni batili kwa kuwa unakiuka mchakato mzima wa udahili ambao hufanywa na vitivo vinavyotakiwa kuhakiki fomu za mwombaji na kuangalia vigezo, vikiwemo ufaulu wa mwanafunzi katika matokeo ya kidato cha sita au sifa zinazofanana na hizo.

Imeongeza kuwa mwanafunzi akishapata udahili, husajiliwa na si kwamba kinachofuata ni udahili mwingine kama inavyofanyika sasa na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha utaratibu na kinalenga kuwaumiza wanafunzi, hasa watoto wa masikini.

Karibu theluthi mbili ya wanafunzi waliorejeshwa nyumbani baada ya chuo hicho kufungwa kutokana na mgomo wa kupinga sera ya uchangiaji gharama za elimu, hawataweza kuendelea na masomo baada ya kutokamilisha masharti ya kurejea chuoni, ikiwa ni pamoja na kulipa sehemu ya ada yao katika kuchangia gharama za masomo.


No comments: