Wednesday, January 14, 2009

Mganga wa jadi anaswa na orodha ya majina ya albino

MGANGA mmoja wa jadi wilayani Chamwino amekamatwa akiwa na orodha ya watu walio na ulemavu wa ngozi (albino).

Mganga huyo alikamatwa na mwenyekiti wa kijiji cha Chinangali ya Pili wilayani Chamwino, Ernest Lesilwa kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji chake.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa mganga huyo pia alikutwa na fomu zaidi ya 29 ambazo anadaiwa kuwa alikuwa akizitumia kuwatoza waganga wa jadi Sh3,500 za mchango ambao haukueleweka mara moja ulilenga kufanyia kazi gani.

Kutokana na tukio hilo lililotokea Januari 7 mwaka huu katika kijiji hicho, Mwenyekiti Lesilwa alisema kuwa wanakijiji wake walipata shaka baada ya kuona mganga huyo (jina tunalo) akiwachangisha waganga wa jadi wa kijiji chake bila kutoa taarifa.

Mganga huyo alikamatwa majira ya saa 10:30 siku hiyo ya Januari 7 na alikutwa akiwa na mganga mmoja (jina tunalo) anayedaiwa kwenda kukusanya fedha alizodai ni malipo kwa ajili ya kuwaruhusu waganga kufanya kazi zao.

Hata hivyo, akiwa katika eneo hilo pia mganga huyo alimtaka mwenzake kumwonyesha kiganja chake cha mkono ili kubaini iwapo kina alama za "M", jambo lililomfanya mganga huyo wa kijijini kuhoji iweje amsome mkono wake.

"Tulipomkamata tulimpekua katika ofisi ya kijiji na cha kushangaza tulimkuta na kichwa kibichi cha nyoka, kitabu cha Koran, msahafu mmoja, simu aina ya Nokia na chaja yake na fomu 29 za kuchangisha waganga," alisema mwenyekiti huyo.

Pia mwenyekiti huyo anadai kuwa ameshangazwa na kitendo cha baadhi ya waganga wa jadi wa kijijini kwake kukubali kumchangia mtaalamu mwenzao huyo wa tiba, bila ya kujali kama ana vibali vya kufanya hivyo.

Waganga wengine wa jadi wa kijiji cha Chinangali wanaodai kutapeliwa na mganga huyo ni pamoja na Grace Mhukula na Agness Lukuna ambao wanadai walitoa Sh3,500 kila mmoja, ingawa mwenyekiti alipomtaka kuonyesha vibali alitoa nakala.

Wakati wakiendelea na mahojiano hayo mganga huyo alianza kutafuna dawa zake za kienyeji na awali alieleza kuwa ni makosa kutekeleza majukumu yake bila kuwasiliana na uongozi wa kijiji.

Tukio hilo limetokea katika kipindi hiki ambacho kuna hekaheka kila mahali nchini juu ya unyama mkubwa wanaofanyiwa walemavu wa ngozi nchini, wengi wao wanadaiwa kukatwa baadhi ya viungo vyao ili vitumike kwa imani za kishirikina.

Juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Omary Mganga hazikufanikiwa, lakini taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani hapa zilithibitisha kukamatwa kwa mganga huyo.

Habari hii imeandikwa na Michael Uledi na kuchapishwa katika gazeti la mwananchi....


No comments: