Kambi ya Upinzani Bungeni imekanusha kuwepo kwa mpasuko ndani ya kambi hiyo. Naibu Kiongozi wa upinzani bungeni Dr. Wilbrod Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema amesema kuwa kambi hiyo bado ipo imara na inauongozi madhubuti.
Akizungumza mjini Dodoma, Dr. Slaa amesema kuwa tofauti zilizopo ni za kawaida kwani kila chana kina mikakati yake hususan ya kisiasa. "Vyema watu wakatofautisha baina ya chama cha siasa na kambi ya upinzani..... kwani tofauti ni kwamba wakiwa ndani ya bunge huendeshwa kwa sheria zaidi wakati nje ya ukumbi wa bunge siasa hutawala," ameeleza Dr. Slaa.
Alieleza kuwa matatizo baina yao hayawezi kuepukika ila kinachofanyika zaidi ni mazungumzo baina yao ili kuzitatua tofauti hizo.
Dr. Slaa amesema kuwa Chadema kitaendeleza ushirikiano wa kisiasa na vyama vya CUF na UDP bali kamwe Chadema hakitaendeleza uhusiano wa mashirikiano na vyama vya siasa vya upinzani vya NCCR-Mageuzi pamoja na TLP.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wameeleza mgawanyiko unaoweza kutokea katika ushirikiano wa vyama hivyo vya upinzani hususan dalili za kuvunjika kwakwe zilizoanza kujitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Tarime.
Dalili hizo za kutoshirikiana pia zilijitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbeya Vijijini ambapo mbali na vyama hivyo kutoafikiana kuweka mgombea mmoja, CUF ilidiriki kuweka pingamizi dhidi ya mgombea wa Chadema.
Akizungumzia suala hilo Dr. Slaa amesema kwa sasa vyama vya CUF, Chadema na UDP vinaendelea na mchakato wa mazungumzo yatakayowezesha kuafikiana jinsi ya kugawana majimbo kulingana na nguvu ya chama husika.
Hata hivyo Dr. Slaa pamoja na kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Hamad Rashid Mohammed wameeleza matumaini yao kuwa ikiwa sheria mpya ya vyama vya siasa itapitishwa na bunge, itatoa nafasi kwa vyama hivyo kuteua mgombea mmoja bila kuathiri mfumo wala itikadi zao.
No comments:
Post a Comment