Makamba atamba, aonya makatibu
Jumatano, 26 Mei 2010 08:47
Habel Chidawali, Dodoma
KATIBU mkuu wa CCM, Yusufu Makamba amewaonya makatibu wa siasa na waenezi wa chama hicho, akiwataka kutonunuliwa na wagombea ubunge na akajinasibu kuwa yeye ni mtu anayekwenda na wakati hivyo hawezi kung’olewa katika nafasi hiyo.
Makamba alitoa onyo hilo jana kwenye ukumbi wa NEC Mjini hapa wakati akifungua semina ya siku tatu kwa makatibu hao ambayo itamalizika kesho.
Makamba, ambaye anajulikana kwa ucheshi, pia aliwasimamisha kwenye mkutano huo baadhi ya viongozi wa jumuiya ya wazazi wa mikoa ya Tanga, Morogoro na Dar es salaam, akiwatuhumu kuwa ni vibaraka wa wagombea ubunge.
Katika hotuba yake, Makamba alitamba kuwa njia itakayomuokoa yeye asing’oke katika nafasi yake ni uamuzi wake wa kusoma kwa bidii.
“Mimi nimesoma na ninasoma kila wakati ndiyo maana sibabaiki kabisa... hata ukiniuliza jambo lolote naweza kukuambia kutokana na ukweli kuwa ninakwenda na wakati na nitaendelea kuwa hivyo kila mara ndio maana watu wanasema kuwa ning’atuke, lakini wanaishia kutokuwa na majibu kwa kuwa ninaenda na wakati," alitamba Makamba ambaye watu walitaka aondolewe baada ya CCM kuanguka kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime.
Aliwataka Makatibu hao kutumia muda wote wa kazi zao katika kupitia vitabu mbalimbali vikiwemo vitabu na vijarida vilivyoandikwa mambo ya CCM ili kujiimarisha katika misingi mizuri ya kupambana na maswali yanayotoka upande wa wapinzani.
Makamba, ambaye amekuwa akimnadi Rais Jakaya Kikwete kuwa ndiye mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho, aliwataka viongozi hao kutokuwa vibaraka wa wagombea ubunge.
Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, mtendaji huyo mkuu wa chama tawala alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni "ushindi ni lazima ndani ya CCM" na kwamba hilo lazima itekelezwe chini ya usimamizi wa makatibu hao.
“Kwa hiyo mkiondoka hapa msiende kulala; hakikisheni chama kinashinda kweli maana hata tafiti mbalimbali zilizofanywa zimeonyesha kuwa CCM inakubalika kwa asimilia kubwa,” alisema Makamba.
Alisema kuwa mbali na utafiti ambao umeonyesha kuwa Kikwete anakubarika kwa asilimia 85.5, uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana ulikuwa ni kipimo tosha cha kuonyesha kuwa CCM inakubalika baada ya kushinda kwa asilimia 91.7.
Source:http://mwananchi.co.tz
S
No comments:
Post a Comment