Wednesday, May 26, 2010
Mo Ibrahim kumtangaza rais bora Afrika 2010
Taasisi ya Mo Ibrahimu inatarajia kumtangaza kiongozi bora mstaafu barani Afrika kwa mwaka 2010 ambaye alichaguliwa kidemokrasia na akaiongoza nchi yake kwa kwa mafanikio katika misingi ya utawala bora.
Kiongozi huyo atajulikana Juni 14 na atakuwa wa tatu kufanikiwa kupata tuzo hiyo inayoandamana na donge nono la papo hapo la dola 5 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh7.3 bilioni za Kitanzania).
Tanzania ina marais wastaafu wawili, Benjamini Mkapa aliyeongoza serikali ya awamu ya tatu (1995-2005) na Ali Hassan Mwinyi, awamu ya pili (1985-1995).
Kwa mujibu wa taarifa Ilioyotolewa na taasisi hiyo Jumatatu wiki hii, rais huyo bora mstaafu wa Afrika atatangazwa mjini London, Uingereza na kamati ya Mo Ibrahim inayoundwa na watu saba waliowahi kuongoza taasisi za kimataifa.
Miongoni mwa wanakamati hao yumo Salim Ahmed Salim aliyewahi kuwa waziri mkuu na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ya Afrika (OAU).
Licha ya kiongozi huyo kutunukiwa fedha hizo taslimu, taarifa hiyo inaeleza kwamba maisha yake yote atakuwa akipewa dola 200,000 za Kimarekani (sawa na takriban Shmilioni 260,000 za Kitanzania).
Kiongozi huyo atakuwa ni wa tatu kutunukiwa tuzo hiyo Barani Afrika tangu taasisi hiyo ilipoundwa mwaka 2007.
Waliotunukiwa tuzo hiyo ni rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano aliyetunukiwa mwaka 2008 na Festus Mogae wa Bostwana (2007).
Mwaka jana kamati hiyo, iliyo chini ya katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, haikumpata mshindi wa tuzo hiyo.
Taasisi hiyo inaongozwa na mfanyabiashara tajiri wa Sudan, Mo Ibrahim, ambaye amebuni tuzo hiyo kwa lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora Barani Afrika.
Story na Leon Bahati
Source:http://mwananchi.co.tz
Jumatano, 26 May 2010 08:48
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment