Monday, March 30, 2009

Sita TRL wakamatwa

Wafanyakazi sita wa shirika la reli TRL wanashikiliwa na polisi kuhusiana na ajali ya treni iliyotokea eneo la Msagali katikati ya stesheni ya Gulwe na Igandu wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Wnaoshikiliwa ni pamoja na wakuu wa stesheni hizo mbili, dereva wa treni ya mizigo, pamoja na wasaidizi wake watatu.

Serikali imetoa siku tatu kuanzia leo kwa mkuu wa idara ya polisi katika shirika hilo kutoa maelezo ya kina juu ya mazingira yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo. Manzingira ya awali yanaonyesha kuwepo kwa uzembe pamoja na hujuma uliosababisha kutokea kwa ajali hiyo.

Ajali ya Treni Msagali Mkoani Dodoma

Sehemu ya behewa lililoharibika....
Jamaa wakikata bodi la behewa ili kunasua miili sita iliyokuwamo ndani...
Kipande cha behewa kilichominywa......
Behewa la mizigo lililogongwa....hii treni ya mizigo ilisimama eneo lisilo na stesheni.....ikadaiwa injini iliharibika......dereva wake hakuweka alama yeyote kuonyesha ishara ya ubofu......hakutoa taarifa haraka kwa mkuu wa stesheni alikotoka au anakoenda...Jamani maswali mengi kuliko majibu...!!!!
Injini ya treni ya abiria iliyogonga treni ya mizigo......

Friday, March 27, 2009

JK abadilisha safu ya wakuu wa wilaya

Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika safu ya Wakuu wa Wilaya nchini ambapo amewateua 15 wapya, kuwastaafisha saba, kuwabadilisha vituo vya kazi wakuu 54 wa wilaya na wawili wakiwekwa benchi wakisubiri kupangiwa kazi nyingine.

Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa ni Bi. Mercy Silla (Arumeru, Arusha), Bw. Norman Sigalla (Hai, Kilimanjaro), Col. Issa E. Njiku (Misenyi, Kagera), Bi. Angelina Mabula (Karagwe, Kagera), Dkt. Rehema Nchimbi (Newala - Mtwara), Francis Isaac (Mbulu, Manyara), Lt. Col. Benedict K. Kitenga (Rorya, Mara) na Lt. Col. Cosmas Kayombo (Mbarali, Mbeya).

Wengine ni Bw. Christopher Ryoba Kangoye (Kwimba, Mwanza); Bi. Queen Mwanshinga Mlozi (Ukerewe, Mwanza); Bi. Fatuma Mwassa (Mvomero, Morogoro); Bi. Fatma Ally (Nanyumbu, Mtwara); Bw. Juma Solomon Madaha (Tunduru, Ruvuma); Bw. Anatory Choya (Kishapu, Shinyanga) na Bw. Erasto Sima (Korogwe, Tanga).

Waliostaafishwa ukuu wa wilaya (vituo vyao kwenye mabano) ni Bw. Elias Maarugu (Misenyi, Kagera); Bw. Deusdedit Mtambalike (Muleba, Kagera); Bw. David Holela (Babati, Manyara); Bi. Hawa Ngulume (Mbarali, Mbeya); Bw. Mashimba H. Mashimba (Kyela, Mbeya); Col. Peter Madaha (Nyamagana, Mwanza) na Bw. Gilbert Dololo (Kibaha , Pwani).

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) inaonyesha kuwa Wakuu wa Wilaya wawili, Bw. Patrick Tsere aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala (Dar es Salaam) na Bi. Doreen Kisamo aliyekuwa Uyui (Tabora) wamewekwa bench na watapangiwa kazi nyingine.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi (Lindi) Bw. Martin Shigela kwa sasa ni Katibu Mkuu wa UVCCM wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai (Kilimanjaro) Bi. Husna Mwilima ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa UWT.

Sunday, March 22, 2009

Magereza watunukiwa nishani

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza, Augustino Nanyaro akimvisha Nishani ya Utumishi Uliotukuka, SSP Kimangano Kivaria wakati wa sherehe fupi ya kutunuku nishani kwa askari na maafisa 301 wa jeshi la Magereza iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu la Isanga mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.


Hapa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza, Augustino Nanyaro akiwapongeza baadhi ya askari magereza baada ya kuwavisha nishani.

Thursday, March 19, 2009

Yako wapi Maisha bora kwa kila Mtz...?

Mwanamama katika kitongoji kimoja mjini Dom akitoka kuteka maji ..... kangani kuna maandishi ya Ari Mpya Nguvu Mpya na Kasi Mpya....... zilotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005..... Yako wapi maisha bora kwa kila mtz....? Alihoji mwanamama mwenzie aliyekuwapo nyuma yake baada ya kuniona 'nikimfotobita.....'

Ni kutokuelewa au ukaidi tu...?

Pikipiki ikiwa imeegeshwa eneo ambalo sio egesho katika stesheni la treni mjini Dom.....jamani hii ni ukaidi au kutoelewa.....??

Wednesday, March 18, 2009

malya ahukumiwa miaka 3 jela

Deus Malya akisindikizwa rumande mara baada ya mahakama mjini Dodoma kumtia hatiani kwa makosa mawili ya kuendesha gari kwa uzembe na mwendo kasi na kusababisha ajali iliyosababisha kifo pamoja na kuendesha gari bila leseni. Kwa kosa la kwanza amehukumiwa miaka mitatu wakati kosa la pili ni mwaka mmoja jela. Adhabu hizo mbili zinakwenda pamoja.


Malya alikuwa pamoja na marehemu Chacha Wangwe wakati gari walimokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam lilipopata ajali eneo la Pandambili kiasi cha Kilomita 120 kutoka mjini Dodoma.

Tuesday, March 17, 2009

Hii ya MU7 kiboko.....

Hii ya Mu7 nimekutana nao kwa mdau mzee wa simulizi...... ila hii hapa ya mwana Afrika Mashariki mwenzetu kiboko.... manake kwanza yupo kivulini chini ya mti... afu sa mwamvuli wanini tena...?? au kunguru wa zenji nini?

Thursday, March 12, 2009

Mbunge wa Busanda afariki dunia

Mbunge wa Busanda kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Kabuzi Faustine Rwilomba amefariki dunia nchini India alikokuwa akitibiwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge, Marehemu Rwilomba alizaliwa tarehe 15 Mwezi Juni 1952 na kupata elimu ya msingi katika shule za msingi Kabugozo 1964-1968 na baadaye Chewamba 1968- 1970.

Marehemu Rwilomba alipata elimu ya sekondari katika shule ya Nsumba 1971-1974 na baadaye kujiunga na chuo cha ualimu cha Korongwe ambapo alipata mafunzo ya daraja la IIIA mwaka 1975 -1976 na kutunukiwa cheti.

Alijunga na Chuo cha Ualimu Butimba mwaka 1981-1983 ambapo alipata Stashahada ya ualimu ya Sanaa (Diploma in Arts) na baadaye Chuo cha Ualimu Morogoro mwaka 1983 -1985 na kupata stashahada ya Elimu (Diploma in Education).

Mwaka 1987-1991 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya kwanza ya Ualimu (B.A in Education) kabla ya kuendelea chuoni hapo na kupata Shahada ya juu ya Uzamiri ya Elimu (M.A in Education) mwaka 1993-1995.

Marehemu Rwilomba alianza kazi kama mwalimu daraja la IIIA katika shule ya msingi Hamuyembe mwaka 1975-1981, kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Nsumba mwaka 1981-1984 akifundisha.

Mwaka 1985-1987 alifundisha katika Chuo cha Ualimu cha Ndala na baadaye kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Butimba mwaka 1991-1992 akiwa Mshauri wa Wanafunzi. Mnamo mwaka 1992-1995 alijuinga na Chuo cha Ualimu Tarime kama Makamu Mkuu wa Chuo na baadaye kuwa Mkuu wa Chuo hicho mwaka 1995-2000.

Aliingia katika ulingo wa siasa mwaka 2000 ambapo alichaguliwa kuwa mbunge hadi mwaka 2005 na kisha mwaka 2005 hadi mauti yalipomkuta.

Globu hii inawapa pole wanafamilia, wanabusanda wote, wabunge pamoja na wanandugu jamaa na marafiki.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi… Amen.

Wednesday, March 11, 2009

UVCCM yaalaani beduli lililomchapa kibao mwinyi

Kijana hili sio jambo la kupuuzia..... lazima uelewe nasafi yenu kama vijana.....
Wadhamini hawa wa uvccm wanoteta na mwenyekiti wa umoja huo kabla ya kutoa tamko rasmi kulaani....

UVCCM imetoa tamko leo mjini Dodoma kulaani kitendo cha kijana mmoja kumdhalilisha rais Mstaafu Alhaji kwa kumzaba kibao…. Baraza la umoja huo limeitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina juu ya mtu huyo na kiini cha kitendo hicho. Aidha baraza hilo pia limikumbusha vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi kwa viongozi wote waliopo madarakani na wastaafu ili kuepusha tendo la aibu kama hilo.

Ikumbukwe wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005, mheshimiwa JK alikumbana na dhahma kama hii pale mjini Mwanza ambapo jibaba moja lilijipenyeza na kuwapita wanausalama na hatimaye kutinga jukwaani na kutaka kuleta kizaazaa.

Kichapo cha beduli......

Hii ni sawa sawa kwa beduli kama hili....
Hiki kichapo kwa huyo jamaa anayedaiwa kufanya kitendo cha aibu cha kudiriki kumchapa kibao rais mstaafu... nimezinyaka kwa mwanafyale.........nikaona niweke picha bee kuonyesha msisitizo.....

Monday, March 9, 2009

mwanafunzi auawa....

Polisi wakichukua mwili wa Marehemu Willy Nyange(17) ambaye alikutwa ameuawa huku akiwa na majeraha kichani katika eneo la uwanja wa Shule ya sekondari Central mjini Dodoma.

Ubunifu ndo huu..

Nauli zimepanda sasa hivi kila mmoja anabuni usafiri wake ili aokoe gharama pichani wanaonekana wakazi wa chanika wakiwa katika pikipiki yenye matairi matatu, watu wengi waliishangaa kutokana na muundo wake.

Mwananchi -9/17/2008

Saturday, March 7, 2009

Polisi wanasa bangi.....

Polisi wakikagua bangi hiyo......

Basi lenyewe ndo hilo....
Polisi wa kituo cha Kati mjini Dodoma wakikagua bangi baada ya kukamata gunia tano za bangi zilizochanganywa na mkaa, kisha kufungwa vyema na kupuliziwa marashi. Bangi hiyo ilikamatwa Jumanne wiki hii katika basi la Najimunisa lililokuwa likitoka mkoani Mwanza kuelekea Dar es Salaam. Watuhumiwa watatu wanashikiliwa na polisi akiwemo Kondakta wa basi hilo na abiria wawili.

Ndo zetuu.....!!!

Watoto wakiwa wamepakizana katika baiskeli mjini Dodoma jana katika staili ya aina yake bila kujua madhara yanayoweza kuwapata ikiwemo ajali.

Friday, March 6, 2009

Ushikwapo shikamana.....!!!!

Aliimba Jumbe......Penzi ni kikohozi kulificha huliwezi......!!!!

Marehemu Uledi azikwa leo

Waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Marehemu Michael Uledi mjini Dodoma leo. Marehemu Uledi amezikwa leo kijijini kwao Buigiri nje kidogo ya mji wa Dodoma.


Thursday, March 5, 2009

Michael Uledi katutoka....

Mwandishi wa habari wa Magazeti ya Mwananchi katika kituo cha Dodoma Michael Uledi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Mirembe alipokuwa amelazwa baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Marehemu Uledi ambaye ameugua TB kwa muda mrefu alizaliwa mnamo mwaka 1969 katika Kijiji cha Buigiri wilaya ya Chamwino.

Marehemu ambaye ameacha Mke na mtoto mmoja atazikwa kesho Ijumaa kijijini kwao Buigiri.

Marehemu Uledi alisoma katika shule ya msingi Buigiri 1977-1983 na baadae mwaka 1986 alijiunga katika shule ya Sekondari ya Chidya wilaya ya Masasi ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1989.


Taarifa za kifo cha Uledi zilitolewa jana na Mke wa marehemu Agness Mzola baada ya kufika hospitalini na kuambiwa kuwa Maiko alikuwa amefariki dunia na ndipo alipoanza kutoa taarifa kwa ndugu na wahusika wa karibu na marehemu.

Mwaka 1990 alijiunga na shule ya sekondari ya Moshi kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita ambako alimaliza mwaka 1992 na baadae alijunga katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa mkoani Mara ambako alihitimu na kasha alikwenda Jijini Dar Es Salaamu ambako alifanya kazi katika makampuni ya watu binafsi kwa kipindi cha miaka miwili.

Uledi alijiunga na MAMET kwa ajili ya kozi ya Uandishi wa Habari kwa muda wa miezi mitatu na alipomaliza alijiunga na shirika la IPP mwaka 1998 ambapo alipangiwa kituo cha Dodoma akiwa ni Mwandishi wa magazeti ya Nipashe na Gadiani pamoja na Radio One.

Alijiunga na chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kilichopo mjini Dodoma mwaka 2001 hadi 2003 ambapo alimaliza Shahada ya juu ya Mipango na Maendeleo Vijijini na kufanya kazi kwa muda mfupi katika shirika la Viwanda Vidogo mkoani Dodoma (SIDO) na baadae alihamishiwa katika kituo cha kazi Mtwara.

Mwaka 2004 hadi 2006 alifanya kazi katika Benki ya Exims katika wilaya ya Masasi akiwa ni Meneja Msaidizi wa Bank na baadae alikaa mkoani Morogoro kwa muda mfupi ambako alikuwa akiandika katika gazeti la serikali la Habari Leo.

Januari mwaka 2007 alijiunga na kampuni ya Mwananchi Communications ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi,Citizen na Mwanasport kazi aliyoifanya hadi mauti yanamchukua.

Alikuwa ni mjumbe katika umoja wa waandishi wa habari za Bunge ambae alikuwa akiwakilisha mkoa wa Dodoma umoja ulioundwa mwaka jana.

Uledi ameacha mke na mtoto mmoja na taratibu za mazishi zinafanyika kwa kushirikiana kati ya kampuni la Mwananchi na ndugu wa marehemu nyumbani kwa Marehemu Nkuhungu mjini Dodoma, mwili wa marehemu unatarajia kusafirishwa leo kwenda Kijijii kwao Buigiri Kilomita 35 kutoka Dodoma mjini ambako mazishi yatafanyika leo saa 5 asubuhi.



Wednesday, March 4, 2009

Polisi yawashikilia wanafunzi wawili Udom

Wanafunzi wakiwa katika moja ya matukio ya migomo katika chuo kikuu cha Dodoma katika picha hii ya maktaba.....

Polisi mjini Dodoma leo imethibitisha kuwakamata wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuhusiana na mgomo uliotokea Jumanne wiki hii chuoni hapo.


Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma (RPC) Omary Mganga amewaambia waandishi wa habari kuwa wanafunzi hao wanaweza kufikishwa mahakamani uchunguzi wa polisi ukikamilika. Hata hivyo alisita kutaja majina ya wanafunzi hao pamoja na makosa ambayo huenda wakashitakiwa dhidi yao.


Amesema kuwa polisi bado inaendelea kukusanya vielelezo juu ya tukio hilo ambapo wanafunzi wanaosoma masomo ya ualimu walifanya maandamano kushinikiza madai yao ikiwamo kulipwa fedha za mkopo wa elimu zinazotolewa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu.


Uharibifu mdogo ulifanywa na wanafunzi hao ikiwemo kuharibu milango ipatayo tisa na kumjeruhi mwangalizi mmoja wa mabweni yao.


Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia Mipango Fedha na Utawala Profesa Shabaan Mlacha amesema kuwa bado kamati ya watu watano iliyoundwa kuchunguza vinara wa mgomo huo inaendelea na kazi yake.


Polisi ililazimika Jumanne wiki hii kufyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi hao ambao walikuwa wakiandamana kutoka katika kampasi yao eneo la Ng’ong’ona kuelekea jengo kuu la Utawala lililopo Chimwaga.

Utatuzi wa migogoro

Mbunge wa Same Mashariki,Anna Kilango Malecela(katikati) akiwaongoza mamia ya wanawake wa jamii ya wafugaji wilayani Same juzi, kutoa tamko linalotaka kutumika kwa njia za kijadi kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji badala ya matumizi ya nguvu.Kushoto kwake ni kijana wa Kimasai, Kipintu Sany aliyejeruhiwa wiki mbili zilizopita katika mapigano ya wafugaji na wakulima. Picha ya Daniel Mjema

Bongo wakati mwingine .... Utalijua jiji....!!!

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu (katikati) na rafiki yake Asha Jumbe wakisindikizwa na askari polisi wakielekea kupanda basi la Magereza kuelekea rumande.


Hapa wakiwa ndani ya basi hilo kabla ya kuelekea rumande..... Picha za Kuruthum Ahmed

Deus Malya ajitetea...

Katika Picha hii ya Maktaba anaonekana Deus Malya (kulia) akiwa na wakili wake wakati kesi yake inayoendelea mjini Dodoma. Leo yaliyojiri ndo kama haya......... endelea.....

Mahakama mjini Dodoma imepanga Ijumaa ya wiki hii kuwa ni siku ya mwisho ya kufunga ushahidi kwa kesi dhidi ya Deus Malya aliyekuwamo katika gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe.

Hakimu Mfawidhi, Thomas Simba amekubali ombi la upande wa utetezi na mashitaka kwa mahakama kupanga tarehe ya kufunga kesi hiyo kabla ya mahakama kutoa hukumu.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amekubali uamuzi wa upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea Godfrey Wasonga huku upande wa mashitaka chini ya mwendesha mashitaka wa serikali Neema Mwanda ukiomba kuwasilishwa kwa ufungaji wa kesi hiyo matamshi na sio maandishi ili kuokoa muda.

Akitoa Utetezi wake jana mbele ya Hakimu Simba, Malya amekanusha kuendesha gari lililopata ajali tarehe 28 mwezi Julai mwaka jana na kusababisha kifo cha marehemu Wangwe.

Akijitetea Malya, ambaye alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Umbwe na baadaya kuendelea na masomo ya sekondari na ngazi ya chuo katika chuo cha Mtakatifu Herbert Nairobi Kenya , alisema kuwa hayawahi kuendesha gari, na wala yajawahi kupata ajali ya gari kabla ya hiyo ya Julai 28 mwaka jana.

Akiongozwa na wakili wake, Malya alipinga ushahidi uioltolewa mahakamani na mashahidi nane waliololetwa na upande wa mashitaka huku akiunga mkono ushahidi wa shahidi wa tisa uliotolewa na mtaala kutoka Taasisi ya Usafirishaji ya Taifa.

Malya aliieleza mahakama kuwa ushahidi uiliotolewa mashahidi hao nane hauthibitishi kuwa yeye alikuwa akiendesha gari hilo aina ya Toyota Collora lenye namba za usajili T865 ARM.

Ajali hiyo iliyokea majira ya saa mbili na nusu usiku katika barabara ya Dodoma-Morogoro eneo la Pandambili, Wilayani Kongwa takriban umbali wa kilometa 120 kutoka mjini Dodoma wakati yaye na marehemu Wangwe wakiwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam.

Malya anashitakiwa kwa makosa mawili katika kesi namba TR 103 ya mwaka 2008 ambayo ni kuendesha kwa mwendo kasi na kusabisha ajali pamoja na kuendesha gari bila ya kuwa na leseni ya udereva.

Malya aliunga mkono ushahidi wa mtaalam kutoka NIT uliothibitisha kuwa gari hilo lilikuwa na kasoro katika gurudumu lake kwa kuwa lilikuwa limeongezwa urefu kwa takriban inchi moja jambo ambalo limengeweza kusababisha gurudumu hilo kupasuka na kusababisha ajali.

Amesema maelezo ya mtaalam huyo yanakinzana na ripoti ya mkaguzi wa gari kutoka idara ya usalama barabarani ambaye aliiambia mahakama kuwa gari hilo halikuwa na ubovu wowote kabla ya ajali.

Malya aliyedai kuwa na umri wa miaka 25 tofauti na ilivyoandikwa kwenye hati ya mashitaka kuwa na umri wa miaka 27 alisema kuwa hati hiyo ya mashitaka inamtaja yeye kuwa na dereva na mfanyabiashara jambo ambalo sio la kweli kwani yeye hamiliki leseni ya udereva na wala hajawahi kuendesha gari.

Kwa mara kadhaa upande wa Mashitaka ulimuomba hakimu kutomruhusu wakili wa utetezi kuuliza maswali yanayolenga kutoa mwelekeo wa majibu ya mteja wake, jambo ambalo hakimu Simba alilitolea ufafanuzi.

Kwa muda mwingi wa utetezi wake, Malya aliieleza mahakama juu ya mashaka aliyonayo katika ushahidi uliotolewa dhidi yake huku akidai kuwa vielelezo kadhaa vilivyowasilishwa mahakamani hapo vinamapungufu.

Malya alieleza mahakama kuwa ripoti mbili zinakinzani kutokana na ukweli kwamba ripoti ya uchunguzi wa maini na figo za marehemu iliyosainiwa na mkemia mkuu inaonyesha kuwa alikuwa amemeza dawa za malaria tofauti na ile ya hospitali ya taifa ya muhimbili ambayo ilionyesha tofauti.

Malya pia amedai mahakamani hapo kuwa ripoti ya mkemia inaonyesha kuwa uchunguzi wa maini na figo za marehemu ulifanywa tarehe moja mwezi Januari mwaka jana, muda ambao marehemu Wangwe alikuwa bado yu hai.

Hata hiyo Hakimu Simba alisita kuruhusu ripoti hiyo kutumika kwa wakati huo katika mahojiano kwani ilipokelewa mahakamani hapo wakati wa usikilizaji wa awali wa kesi hiyo kama kielelezo kisichokuwa na pingamizi.

Kesi hiyo ambayo imevuta hisia za wakazi wengi wa Dodoma , Hakimu Simba pia alitoa maelekezo mara kadhaa juu ya utaratibu wa utetezi wa tafsiri kadhaa za masuala yaliyojitokeza mahakamani hapo.

Malya aliieleza mahakama kuwa alimfahamu Marehemu Wangwe kupitia baadhi ya viongozi wa Chadema ambao amekuwa akiwafanyia kazi zao kadhaa zihusianazo na uchapishaji na ubunifu wa maandishi na michoro.

Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza alimfahamu marehemu Wangwe mwaka 2005 wakati alipomfanyia kazi ya kubuni na kutengeneza vipeperushi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi na pia fulana kwa ajili ya kutunisha mfuko kwa ajili ya maendeleo ya jimbo la Tarime.

Malya aliieleza mahakama kuwa alifika mjini Dodoma baada ya kuitwa na marehemu Wangwe kwa ajili ya kazi ya kuhariri na ubunifu wa maandishi wa kitabu chake kilichokuwa na jina la “Hii si Demokrasia”.

Siku hiyo ya ajali, alieleza kuwa walianza safari majira ya saa moja usiku na baada ya kutoka nje kidogo ya mji, walisimama ambapo marehemu alikwenda kununua kadi ya muda wa maongezi wa simu ya mkononi.

Alisema marehemu alimsihi akae katika kiti cha nyuma ili aweze kulala kwani alikuwa anajisikia usingizi, jambo ambalo alikubali na kwenda kukaa kiti cha nyuma ya dereva na kufunga mkanda wa usalama katika gari.

“Baada ya kwenda mwendo mrefu kidogo, ghafla nilisikia marehemu akisema hayaaaa…..!! na mara gari likaanza kubingirita na baada ya kutulia ndipo nikashituka kuwa tumepata ajali,” alieleza Malya.

Alipoulizwa na Hakimu, Malya alieleza kuwa mwili wa marehemu wangwe ambaye alidai kuwa ndiye aliyekuwa akiendesha gari huku hajafunga mkada wa usalama garini ukiwa umelala sehemu ya mbele ya gari, miguu yake ikiwa upande wa dereva wakati sehemu nyingine za mwili zikiwa upande wa pili huku koti lake likiwa limebanwa.

Ubishani mdogo ulizokuwa unatokea wakati wa mahojiano baina ya Malya na upande wa mashitaka ambao ulimtaka mshtakiwa huyo kujibu Ndiyo ama Hapana kwa maswali aliyokuwa akiulizwa huku Malya akitaka kutoa ufafanuzi wa hayo aliyokuwa akiulizwa.

Tuesday, March 3, 2009

Angalia makini kabla ya kukaa kwa raha zako....

Kabla jamaa hajakaa tu..... snake kaibuka ......
Baada ya purukushani kidogo..... snake kaficha kichwa.....
Mshkaji akaona isiwe tabu..........

Titanike lingine......

hii hapa kwa ndani sehemu ya kupumzikie.....
muonekano wake kwa nje....